Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) imeshika nafasi ya pili katika tuzo ya utendaji bora na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kama sehemu ya mchango wake katika uwezeshaji wananchi kiuchumi na utendaji bora wa mfuko huo.
Kabla ya kutoa tuzo hizo kwenye kongamano la Saba la uwezeshaji wananchi kiuchumi, Jijini Dodoma, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amezipongeza Taasisi na Sekta zote binafsi zinazo jishughulisha na uboreshaji wa Maisha ya wananchi kiuchumi na kuwa huko nikuunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Waziri Mkuu Majaliwa, ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya Maliasili na Utalii ili kujiendeleza kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Katibu Tawala Mfuko wa Misitu Tanzania, Dkt. Tuli Salum Msuya ameishukuru NEEC kwa kutambua mchango wa TaFF katika kuwezesha wananchi kiuchumi na kutambua utendaji bora wa Mfuko huu hali iliyopelekea kupewa tuzo.
Dkt. Msuya ameendelea kusema kuwa tuzo hiyo ni kichocheo cha utendaji kazi zaidi kwa Mfuko huo ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na fursa zilizopo katika sekta ya Misitu na kuchangia zaidi katika pato Taifa.
Aidha Dkt. Msuya ameongeza kuwa TaFF hutoa ruzuku kwa lengo la kuwezesha miradi ya kuboresha uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali misitu hapa nchini.
Wafanyakazi wa Mfuko wa Misitu Tanzania wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kupokea na kushangilia ushindi wa pili wa utendaji bora kutoka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) katika chumba cha mikutano ofisi za TaFF Dodoma. Kwenye picha ni Katibu Tawala aliyevalia koti jeupe akiongoza timu ya ushindi.
Kwa picha zaidi tembelea: https://www.mfukowamisitu.go.tz/index.php/resources/photos